Leviticus 23:24-44

24 a“Waambie Waisraeli: ‘Katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba mtakuwa na siku ya mapumziko, kusanyiko takatifu la ukumbusho litakaloadhimishwa kwa kupiga tarumbeta. 25Msifanye kazi zenu zozote za kawaida, lakini toeni sadaka kwa Bwana iliyoteketezwa kwa moto.’ ”

Siku Ya Upatanisho

(Hesabu 29:7-11)

26 Bwana akamwambia Mose, 27 b“Siku ya kumi ya mwezi huu wa saba ni Siku ya Upatanisho. Mtafanya kusanyiko takatifu, mfunge, nanyi mtoe sadaka kwa Bwana ya kuteketezwa kwa moto. 28Msifanye kazi siku hiyo, kwa sababu ni Siku ya Upatanisho, ambapo upatanisho unafanyika kwa ajili yenu mbele za Bwana Mungu wenu. 29 cMtu yeyote ambaye hatafunga siku hiyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake. 30 dMtu yeyote atakayefanya kazi siku hiyo nitamwangamiza kutoka miongoni mwa watu wake. 31 eHamtafanya kazi kamwe. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo popote mnapoishi. 32 fNi Sabato ya mapumziko kwenu ninyi, na lazima mfunge. Tangu jioni ya siku ya tisa ya mwezi hadi jioni inayofuata, mtaishika Sabato yenu.”

Sikukuu Ya Vibanda

(Hesabu 29:12-40)

33 Bwana akamwambia Mose, 34 g“Waambie Waisraeli: ‘Katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, Sikukuu ya Bwana ya vibanda itaanza, nayo itaadhimishwa kwa siku saba. 35Siku ya kwanza ni kusanyiko takatifu, msifanye kazi zenu za kawaida. 36 hKwa siku saba toeni sadaka kwa Bwana za kuteketezwa kwa moto. Kwenye siku ya nane fanyeni kusanyiko takatifu, na mtoe sadaka kwa Bwana ya kuteketezwa kwa moto. Ni kusanyiko la mwisho, msifanye kazi zenu za kawaida.

37(“ ‘Hizi ni sikukuu za Bwana zilizoamriwa, ambazo mtazitangaza kuwa makusanyiko matakatifu kwa kuleta sadaka kwa Bwana za kuteketeza kwa moto: sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka, dhabihu na sadaka za vinywaji zitahitajika kila siku. 38 iSadaka hizi ni nyongeza ya zile mnazozitoa katika Sabato za Bwana, na pia ni nyongeza ya matoleo yenu ya chochote mlichoweka nadhiri, na sadaka zenu zote za hiari mnazozitoa kwa Bwana.)

39 j“ ‘Basi kuanzia siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, baada ya kuvuna mazao yote ya nchi, mtaadhimisha sikukuu kwa Bwana kwa siku saba; siku ya kwanza ni mapumziko, pia siku ya nane ni mapumziko. 40 kSiku ya kwanza mtachukua matunda mazuri ya miti, matawi ya mitende, matawi yenye majani mengi, na matawi ya mirebi, nanyi mtashangilia mbele za Bwana Mungu wenu kwa siku saba. 41Mtaadhimisha siku hii kuwa sikukuu kwa Bwana kwa siku saba kila mwaka. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo; iadhimisheni mwezi wa saba. 42 lMtaishi katika vibanda kwa siku saba: Wazawa wote wa Waisraeli wataishi katika vibanda, 43 mili wazao wenu wajue kuwa niliwafanya Waisraeli waishi kwenye vibanda nilipowatoa Misri. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”

44Kwa hiyo Mose akawatangazia Waisraeli sikukuu zilizoamriwa na Bwana.

Copyright information for SwhNEN